Viongozi wa vyama vikuu vya upinzani Uganda, akiwemo Robert Kyagulanyi na Dkt Kizza Besigye wametangaza kuungana kwa ajili ya kumdhibiti rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026.
Viongozi wa upinzani wameeleza kuwa wameweka kando tofauti zao za kisiasa katika harakati ya safari hii na kwamba wameanza kujiandaa mapema ipasavyo na kuwa tayari msimu wa uchaguzi utakapoanza.
Meya wa mji wa Kampala Erias Lukwago ambaye pia ni rais wa chama cha FDC ameelezea kuwa muungano huo ni mwendelezo wa harakati zao za kuikomboa Uganda kutoka katika utawala wa kiimla wa rais Yoweri Museveni.
Habari za viongozi wakuu wa upinzani kutangaza muungano huo zimetolewa wakati wananchi mbalimbali wakiendelea kuwakosoa kwa kuonyesha uchu wa madaraka badala ya kuzingatia maslahi ya taifa.
“Taifa hili ni kubwa kuliko kujenga vyama vyetu vya siasa. Katika nchi ambayo hata chama cha siasa hakiwezi kuendesha shughuli zake hatuwezi kujivunia kuwa vyama vya siasa, kwa hiyo sote ni watumwa na tunapozidi kupigana miongoni mwetu, tunaendeleza utawala wa Museveni,” alisema Rais wa chama cha NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.