Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la maendeleo la Ujerumani GIZ limetoa msaada wa vifaa vya tehama vyenye thamani ya sh Mil 200 kwa hospitali ya Manundu iliyopo Wilayani Korogwe.
Msaada huo ambao unalengo la kusaidia uwekezaji wa miundombinu ya Tehama kwa ajili ya utekelezaji wa afua za afya za kidigitali Kwa ajili ya kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za afya.
Akiongea wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Naibu Meneja Programu kutoka GIZ Erick Msoffe amesema kuwa msaada huo unalengo la kubadilisha taratibu za kiutawala na kiafya katika hospitali hiyo kwa kuondoa matumizi ya kumbukumbu za karatasi.
“Sisi GIZ tunashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuongeza mageuzi haya ya mifumo ya kidigitali kwa hospitali nyingi hapa nchini na hivyo zitaongeza ufanisi na kupunguza makosa katika takwimu lakini na utoaji wa huduma “amesema Msoffe.
Hata hivyo Mganga mfawidhi wa hospitali ya Manundu Dkt Heri Kilwale amesema kuwa tayari wamefanikiwa kufunga Mfumo huo kwa zaidi ya asilimia 95 % .
Hivyo amesema kuwa tayari uwepo wa Mfumo huo umesaidia mafanikio mbalimbali ikiwemo muda wa wagonjwa kupata huduma kwenye hospitali hiyo umeweza kupungua kutoka saa 12 hadi saa tatu na nusu Kwa mgonjwa mmoja.