Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameshauri sheria zinazohusika katika mchakato wa utoaji haki nchini kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuondoa konakona zinazochangia ucheleweshaji wa kumaliza mashauri.
Prof. Juma ametoa ushauri huo katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa wadau mbalimbali wa usuluhishi iliyokuwa imeandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Kuna tatizo kubwa sana katika mfumo wetu wa sheria, kuna michakato mingi, kuna konakona nyingi na kwa bahati mbaya, taaluma yetu ya sheria imejengwa kwa kutegemea hizo konakona,” amesema.
Ameeleza kuwa moja ya maboresho ambayo ni muhimu katika karne ya 21 ni usuluhishi na maboresho hayo yanatokana na ukweli kwamba taratibu za kimahakama pamoja na sheria, zikiwemo zile za mienendo ya madai na jinai, zilitungwa katika maudhui ya karne ya 18 au 19.
“Ndiyo maana kuna wakati mmoja, Profesa kutoka Marekani alikuja nchini na aliposoma sheria yetu ya mienendo ya madai, aliposoma sheria ya mienendo ya jinai, aliposoma sheria ya ushahidi aliandika andiko na kusema zote ni za kizamani,” Jaji Mkuu ameeleza.
“Profesa huyo alibaisha sheria alizopitia zina konakona nyingi ambazo zinaweka fursa za mapingamizi na kuruhusu mdaawa kurudi mahakamani hata baada ya shauri kukamilika na kazi kuanza upya.
“Wenzetu Wizara ya Elimu wameangalia upya mfumo wa elimu, mfumo wa elimu ya sheria hatujauangalia na hata marekebisho ya sheria tunayofanya ni vipande vipande, hatuangalii marekebisho kwa ujumla na ndiyo maana kunakuwa na changamoto nyingi sana,” Prof. Juma amesema.
Hivyo, Jaji Mkuu akasema kuwa pamoja na kuhimiza wananchi kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kuna haja pia ya kuangalia upya sheria zote kwani taratibu zilizopo zinaweka nafasi ya mashauri kuchukua zaidi ya miaka mitano au sita.
“Je, kuna haja ya mgogoro wa ardhi uanzie kata, uende baraza la ardhi, uende Mahakama Kuu na Mahakama Kuu kuna mapingamizi mengi, kuna maombi mengi, uende Mahakama ya Rufani, halafu hapo hapo uwe na Nchi ambayo ni shindani katika biashara na uwekezaji.