Katika operesheni ya kupambana na ugaidi katika jimbo la Benue la katikati mwa Nigeria, vikosi vya kulinda usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kukomboa takriban watu tisa waliokuwa wametekwa nyara na watu wwenye silaha.
Katika taarifa yake ya Alkhamisi, jeshi la Nigeria limetangaza habari hiyo mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa magaidi wawili wametiwa mbaroni.
Sunday Igbinomwanhia, kamanda wa wanajeshi huko Benue, amesema hayo wakati akiwaeleza waandishi wa habari masuala yanayoendelea kwenye mji wa Makurdi ambao ndio makao makuu ya jimbo la Benue na kusema kuwa, kwa uchache watu wawili wenye silaha wametiwa mbaroni wakati wa mapigano ya risasi baina ya jeshi na watu wenye silaha. Amesema, operesheni hiyo imefanyika kwenye msitu mmoja wa jimbo hilo siku ya Jumanne.
Mateka waliokombolewa ni pamoja na wanawake wanane na mwanamume mmoja na walitekwa nyara tarehe 11 Januari wakati walipokuwa wanasafiri kwenye basi la biashara kwenye barabara ya Otukpo-Enugu huko Benue.
Igbinomwanhia pia amesema: “Wakati wa mapigano ya risasi, watekaji nyara walikimbia maficho yao kutokana na mashambulizi makali ya vikosi vya usalama vya Nigeria, kuwaacha mateka hao katika eneo hilo. Amesema, jeshi limefanikiwa pia kuteka silaha na risasi za watu hao wenye silaha.
Vile vile amesema: “Mateka hao walihojiwa baada ya kupokea matibabu na baadaye kuruhusiwa kuungana na familia zao.”