Mamlaka Ecuador imesema watu 2 wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya mwendesha mashtaka aliyekuwa anachunguza uvamizi uliofanywa na genge moja wiki iliyopita katika kituo cha televisheni wakati matangazo yakiwa hewani.
Mwendesha mashtaka huyo Cesar Suarez aliuwawa kwa kupigwa risasi jana akiwa ndani ya gari lake katika mitaa ya mji wa bandari wa Guayaquil ambao ni kitovu cha vita vya madawa ya kulevya kati ya serikali na makundi ya kihalifu yenye nguvu.
Upande wa mwendesha mashtaka umeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, Suarez alikuwa na jukumu la kulitambua genge lililohusika na uvamizi huo katika kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali cha TC.
Rais wa nchi hiyo Daniel Noboa alitangaza nchi hiyo kuwa katika “hali ya vita” baada ya makundi ya uhalifu wa madawa ya kulevya kuanza kampeni ya utekaji nyara na mashambulizi, kama jawabu kwa hatua ya serikali ya kuanzisha kamatakamata ya wahalifu.