Jumuiya ya Kikanda ya Afrika Mashariki ya Maendeleo ya Kiserikali (Igad) imewataka majenerali wanaohasimiana katika vita nchini Sudan jenerali Abdel Fattah al Burhan anayeongoza utawala wa kijeshi mjini Khartoum na kiongozi wa kundi la RSF jenerali Mohamed Hamdan Daglo kukutana ana kwa ana na kuafikiana kusitisha mapigano nchini humo ndani ya siku 14.
Wito huo umetolewa na Jumuiya ya IGAD katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baada mwenyekiti wa jumuiya hiyo ambaye pia ndiye rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh kufanya mkutano wa dharura na baadhi ya marais na viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Mkutano huo uliofanyika kwa faragha katika ikulu ya rais mjini Entebbe nchini Uganda uliitishwa kwa dharura kujadili mada mbili muhimu, ikiwemo vita nchini Sudan pamoja na mvutano wa hivi karibuni kati ya Somalia na Ethiopia kuhusu mkataba wa makubaliano ulisainiwa kati ya utawala wa Wazir mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na jimbo liliojitenga la Somaliland.
Marais wakiwemo William Ruto wa Kenya, Hassan Sheik Mohamud wa Somalia, Salva Kiir wa Sudan Kusini pamoja na mwenyeji wa mkutano huo rais Yoweri Museveni wa Uganda walihudhuria mkutano huo.
Awali serikali ya Ethiopia ilisema haingetuma wawakilishi wowote kwa mkutano huo kutokana na kutoarifiwa mapema kuhusu kikao hicho.