Cameroon inazindua mpango wa chanjo dhidi ya malaria, katika mapambano ya kimataifa yanayotarajiwa kuokoa maelfu ya maisha ya watoto kote barani Afrika.
Chanjo ya RTS,S iliyoidhinishwa na shirika la afya duniani (WHO), iliyotengenezwa na kampuni za dawa ya nchini Uingereza, GlaxoSmithKline (GSK), inalenga kuwafikia watoto wachanga katika wilaya 42 zilizoathiriwa zaidi nchini humo.
Nchi hiyo ya Afrika ya kati itakuwa nchi ya kwanza kutoa dozi za chanjo ya malaria kufuatia kampeni za majaribio zilizofanikiwa nchini Kenya, Ghana na Malawi.
Mpango huo unaotarajiwa kuanza Jumatatu, umetajwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za miongo kadhaa za kukabiliana na ugonjwa wa malaria barani Afrika.
Nchi nyingine 20 zinalenga kuzindua mpango huo mwaka huu, kulingana na muungano wa kimataifa wa chanjo Gavi. Kwa mujibu wa GSK, kuna uwezekano wa kuzalisha takriban dozi milioni 15 za malaria kila mwaka.