Wakati kukiwa na tahadhari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini baaadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yameamua kufanya usafi katika mazingira ya fukwe ya bahari ya Dar es salaam ili kuiunga mkono serikali katika udhibiti wa maradhi hayo hatari kiafya miongoni mwa jamii.
Licha ya mvua kubwa kunyesha majira ya asubuhi jijini Dar es salaam Ayotv imeshuhudia watendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Mugo Foundation wakiongozwa na mkurugenzi ikifanya usafi na kupanda miti katika eneo la ufukwe ambapo Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Chiku Mugo amesema wameamua kuweka mazingira katika hali ya usafi ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kwa kuwa athari yake ni kubwa kiafya na kiuchumi.
Nao baadhi ya washiriki wa tukio hilo la usafi wamesema zoezi hilo ni endelevu kwa kuwa wanatarajia kufika katika mikoa mingine ili kuhakikisha suala la usafi na upandaji miti liwe ni sehemu ya maisha ya kila siku badala ya kutumika katika matukio maalumu pekee.