Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema, watoto zaidi ya 67,000 katika mkoa wa Somali, kusini mashariki mwa Ethiopia, wanashindwa kwenda shule kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El Nino.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu mafuriko katika mkoa wa Somali na athari yake katika sekta ya elimu iliyotolewa jana jumatatu, UNICEF imesema mafuriko hayo yamevuruga huduma za elimu katika mkoa huo kwa karibu miezi miwili kwa kuwa shule zilikuwa zimefungwa.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka UNICEF, mafuriko hayo yameathiri shule 227 katika kanda nne za mkoa wa Somali, ambazo kati yao, 139 zimefungwa na 88 zimeharibika, na kuwafanya watoto 67,000 kushindwa kuendelea na masomo.