Wageni wanaweza kuruhusiwa kujiunga na jeshi la Ujerumani huku Boris Pistorius, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, akijaribu kuajiri wanajeshi 20,000 zaidi kutokana na vitisho kutoka kwa Urusi.
“Hatutakuwa wanajeshi wa kwanza barani Ulaya kufanya hivyo,” Bw Pistorius aliambia gazeti la Tagesspiegel la Ujerumani, huku akithibitisha kuwa wazo hilo lilikuwa likizingatiwa na serikali mjini Berlin.
Chini ya sheria za Ujerumani ni raia pekee wanaoweza kuhudumu katika Bundeswehr kimsingi, ingawa wageni wanaweza kuruhusiwa kujiunga katika kesi fulani maalum, kulingana na Bild, jarida la udaku la Ujerumani.
Tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, Bundeswehr imeongeza juhudi za kuajiri ili kufikia lengo lake jipya la askari 20,000 wa ziada, na mfululizo wa kampeni za matangazo zinazolenga Generation Z, pamoja na mipango ya kuruhusu kazi rahisi.