Baraza la mawaziri nchini Zimbabwe ,limeunga mkono pendekezo la kuondolewa kwa sheria inayoruhusu adhabu ya kifo, hatua ambayo ni muhimu katika juhudi za kufuta sheria hiyo kwenye taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano kwenye taifa hilo Jenfan Muswere, uamuzi wa baraza la mawaziri uliafikiwa baada ya kufanyika kwa mashauriano ya kitaifa.
Iwapo bunge litapiga kura kuidhinisha muswada huo, kifungo cha maisha jela kitatumika kama kifungo cha juu zaidi.
Rais Emmerson Mnangagwa amekuwa akiikashifu sheria hiyo inayopendekeza kifo kwa wahusika ambao uamuzi wa mahakama inawapa hukumu hiyo.
Alihukumiwa adhabu ya kifo mwaka wa 1965 kufuatia tuhuma kwamba alihusika na tukio la kulipua treni wakati akipigana dhidi ya utawala wa wazungu nchini humo.
Adhabu ya kifo nchini Zimbabwe ni mwendelezo wa sheria ya zama za ukoloni na licha ya kuendelea kutumika kwenye taifa hilo, Harare haijatekeleza mauaji tangu 2005 chini ya sheria hiyo.