Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye (@napennauye ) amesema Serikali ya awamu ya sita haijawahi na haina mpango wa kuminya uhuru wa Vyombo vya Habari ambapo amevitaka Vyombo hivyo kuwapa nafasi Wanasiasa wote bila kujali tofauti ya Vyama vyao.
Akiongea Jijini Dodoma leo, Nape amesema “Serikali imeona kuhusu Wasafi FM kuzuia mahojiano kati ya Tundu Lissu na Radio hiyo na maelezo yaliyotolewa yalisema wamezuia kwa maelekezo kutoka juu lakini baadaye nimeona Lissu mwenyewe akisema amepewa taarifa kwamba ilikuwa ni mkanganyiko wa ndani wa Wasafi”
“Serikali inatoa taarifa kwamba toka Rais Dkt. Samia Suluhu ameingia madarakani ameimarisha uhuru wa Vyombo vya Habari na Demokrasia, kilichotokea leo kimetusikitisha hasa kauli kuwa ni maelekezo kutoka juu, Serikali ya Rais Samia haijafanya na haina mpango, tuondokane na hofu ya kujifungia sehemu na kuwa na visingizio kwamba kuna maagizo, kuna Serikali inafanya hivi hapana”
“Nitoe wito kwa Wanahabari, timizeni wajibu wenu kwa kufuata sheria, Serikali haina mpango wa kuingilia uhuru wa Wanahabari kutimiza majukumu yao, kama kuna mahali Watu wanaamua kutumia content yoyote wafanye kwa kufuata sheria lakini hakuna Kiongozi yeyote wa Serikali ambaye ana mpango wa kuingilia uhuru wenu”
“Natoa wito kwa Wasafi hiki kipindi walichokiahirisha wakifanye, Vyombo vyote vya Habari wapeni uwanja sawa Wanasiasa watimize majukumu yao, Mtu akisemwa, wa upande wa pili apewe nafasi ya kujieleza ndio namna ambavyo tutaendesha siasa za Nchi yetu, Rais Samia kupitia 4R zake ameelekeza, tuvumiliane, tufanye maridhiano, na haya ndiyo mambo ya kufanya, na Rais ameonesha kwa mfano, juzi CHADEMA wameomba maandamano wameruhusiwa, Serikali hatuna sababu ya kuingilia uhuru wa Vyombo vya Habari, nampa pole Mjomba wangu Lissu kwa kadhia aliyoipata asubuhi, narudia wapeni uwanja sawa Wanasiasa waongee kwa hoja na hasa tunapoelekea kipindi cha uchaguzi”