Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiagiza Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) kuongeza wigo wa kuwajengea uwezo Wahandisi Washauri nchini ili kuhakikisha utalaam na ujuzi unakuzwa kwa maendeleo ya nchi.
Bashungwa amezungumza hayo jijini Dodoma katika mkutano uliokutanisha Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), na kusisitiza kuweka mikakati mahususi ya uendelezaji wa Wahandisi Washauri kitaaluma ili kukuza tasnia ya Uhandisi.
“Vipaumbele na maagizo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika sekta hii ni kuona ushiriki mkubwa wa Wahandisi na Makandarasi Wazawa katika kazi za ujenzi na usimamizi wa miradi (Local Content), sisi kama wasaidizi wake tuhakikishe tunalitekeleza hili”, amesema Bashungwa.
Aidha, ameelekeza kuhakikisha kunakuwa na uwepo wa ushirikishwaji wa Wahandisi wahitimu katika mpango wa mafunzo kwa vitendo (SEAP) kwenye miradi mikubwa inayotekelezwa nchini ili kuwajengea uwezo.
Vilevile, ameagiza kuangalia maeneo yote yenye changamoto katika Sheria ya Usajili ili kuwawezesha wahandisi kufanya ubunifu na kusaidia nchi katika uchumi wa viwanda na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
“Tengenezeni mazingira wezeshi kwa Wahandisi Washauri wazawa kuweza kushiriki katika miradi ili kuokoa fedha za Serikali”, ameagiza Bashungwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Eng. Aisha Amour, ameishauri Bodi na Manejimenti ya ERB kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi kazini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Menye Manga, ameahidi kushirikiana na Menejimenti ili kuleta mabadiliko chanya katika Taaluma ya kihandisi na kuhakikisha taaluma inaendelezwa na kukuzwa ili kuongeza idadi ya wataalam hao nchini.