Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaasa Wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa zisizo rasmi za macho kwa lengo la kutibu ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes), kwakuwa matumizi hayo yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo itakuwa kwa wengi wa Wagonjwa waliokwisha kupata madhara kwenye kioo cha jicho kwa kutumia vitu hivyo.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo amesema hayo leo Jijini Dar es salaam ambapo amesema ugonjwa wa ‘Red Eyes’ hauleti upofu lakini matumizi ya dawa zisizo rasmi na zinazonunuliwa kiholela yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo inaweza kuwapata baadhi ya Wagonjwa waliopata vidonda kwenye kioo cha jicho baada ya kutumia dawa hizo zisizo rasmi.
Amesema baadhi ya vitu vinavyotumika ni pamoja na dawa zenye vichocheo vya ‘steroids’ ambazo Wananchi wanakwenda kununua wenyewe kwenye maduka ya dawa, tangawizi, chai ya rangi illiyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yakitumika wakati wa janga la Covid – 19, maji ya chumvi na maziwa ya Mama, ambavyo vitu vyote hivyo sio salama na havijaelekezwa na Wataalamu.
Wizara imeendeleza kusisitiza Jamii kuzuia kuenea kwa maambukizi haya kwa kuzingatia usafi binafsi na kanuni za afya ikiwa ni pamoja na usafi wa mikono na uso, kuzuia kugusa macho , kunawa mikono na maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara, kuzingatia kutokushikana mikono maeneo ya sehemu za ibada, kutumia taulo au leso za karatasi kufuta tongotongo au machozi na kufika kwenye kituo cha kutolea huduma pale Mtu apatapo dalili za Red Eyes