Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni lazima kufanya jitihada za dhati kukabiliana na uharibifu wa mazingira ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kuhamasisha utunzaji wa mazingira lililofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume iliyopo Unguja – Zanzibar. Amesema suala la mazingira linagusa sekta zote muhimu za kijamii hivyo ni jukumu la kila mtanzania kuunga mkono juhudi za kuhifadhi mazingira.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi kuepuka kukata miti ovyo, kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa, kuacha kuchafua mazingira Pamoja na uchimbaji wa mchanga katika maeneo yasiyo rasmi. Amezitaka kila Taasisi na Wizara kuhakikisha zinapanda miti katika maeneo yao.
Amesema unahitajika ushirikiano baina ya watanzania wote kuhakikisha miti inapandwa ili kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Pia amesisitiza umuhimu wa vijana hususani wanaopata elimu vyuoni kupanda miti na kuitunza katika maeneo ya vyuo Pamoja na makazi.
Makamu wa Rais amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kutoa elimu, kuandaa mipango ,kuboresha sera na sheria zinazohusu mazingira ikiwa ni Pamoja na kuhamasisha wananchi kuwa sehemu ya kuhifadhi na kutunza mazingira.
Pia amemuelekeza Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha programu ya utunzaji Mazingira ya Green Legacy iliyolenga kukabiliana na uharibifu wa Mazingira kwa kupanda miti.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano baina ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume – Zanzibar Pamoja na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) ili kubadilishana ujuzi na maarifa.