Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema serikali kupitia wizara ya afya imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kidigitali ili kuwezesha na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ameyasema hayo tarehe 8 Februari, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga na Kituo cha Afya Mazwi katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Dkt. Magembe amesema kwa mara ya kwanza mkoani humu Serikali imeweza kununua mashine mpya ya kisasa CT-scan na tangu kufungwa kwa mashine hiyo mwezi Desemba 2022 hadi leo imeweza kuhudumia wagonjwa takribani 96.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ili watanzania wapate huduma bora, kwa mara ya kwanza katika historia ya mkoa huu ameweza kununua mashine mpya ya kidigitali ya CT- Scan ambayo imeanza kuwahudumia wagonjwa mbalimbali kama vile wahanga wa ajali, wenye matatizo ya Uti wa Mgongo, kiharusi na magonjwa mengine ya viungo vya ndani hadi kufika leo wamefika takribani wagonjwa 96” Amesema Dkt. Magembe.
Amesema kuwa Kwa sasa Hospitali hiyo inawapiga picha wa 4 ila bado hakuna msomaji na hivyo picha hizi zinatumwa kidigitali kwenda Hospitali ya Kanda Mbeya na majibu yanarudi ndani ya masaa 2 hadi 6, jambo ambalo limewezeshwa na uamuzi wa Mhe Rais Dkt Samia baada ya kununua mashine za kidigitali kama sehemu ya mkakati mmoja wapo wa kukabiliana na upungufu wa watumishi nchini.