Mwanariadha wa Kenya, anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio ndefu na aliyekuwa akipewa nafasi katika mashindano yajayo ya Olimpiki jijini Paris, Kelvin Kiptum, amefariki dunia katika ajali ya gari, magharibi mwa nchi hiyo, polisi wamethibitisha.
Kwa mujibu wa polisi, mwanariadha huyo alikuwa akiendesha gari yake kutoka Kaptagat kuelekea Eldoret maajira ya saa tano usiku hapo jana kabla ya kupinduka na kumuua yeye pamoja na kocha Wake raia wa Rwanda, Gervais Hakizimana.
Kiptum, alijipatia umaarufu mwishoni mwa mwaka jana mwezi Oktoba, baada ya kuweka rekodi kwenye mbio za Chicago, akimaliza kwa kutumia muda wa saa 2 na sekunde 35, akipiku rekodi ya mkenya mwenzake Eliud Kipchoge ya sekunde 34.
Mbio za Chicago, ilikuwa ni mara yake ya tatu kushiriki katika mbio ndefu akiwa na umri wa miaka 23, akishinda mbio za Valencia mwaka 2022 na London mwaka uliofuatia, na alikuwa ameahidi kujaribu kukimbia katika mbio rasmi na kumaliza ndani ya saa 2.