Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni.
Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania. Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam.