Hii leo ni siku ya redio duniani ambapo Umoja wa Mataifa unamulika nafasi ya chombo hicho kilichobuniwa takribani karne moja iliyopita katika kukuza na kujenga amani wakati huu ambapo pia ni miaka 75 tangu kuanzishwa kwa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa mwaka huu ni radio na amani ambapo Mkuu wa mawasiliano ya kimkakati kwenye Idara ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa amani Francesca Mold amesema maadhimisho ya sasa yamekuja wakati muafaka zaidi kwani Umoja wa Mataifa umeanza kampeni yam waka mmoja kuelekea kilele miaka 75 tangu kuanza kwa operesheni za ulinzi wa amani.
Radio ni mawasiliano ya umma ambayo yanawafikia kundi kubwa la wasikilizaji ulimwenguni kote. Bado inatambulika kuwa ni chombo cha mawasiliano chenye nguvu ya ushawishi na kinatumia gharama ndogo zaidi.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa radio iliandaliwa kuzifikia jamii zilizo katika maeneo yaliyoko kando ya miji na vijiji, ambavyo haviwezi kufikiwa kwa urahisi kutokana na matatizo ya barabara na usafiri.
Hizi ndizo jamii ambazo zinaathirika zaidi na matatizo mbalimbali. Jamii hizi zinamakundi kama vile, waliokosa fursa za elimu, wenye ulemavu, wanawake, vijana na maskini.