Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema Jumatano takriban watu 28,576 wameuawa katika eneo hilo wakati wa vita kati ya wanamgambo wa Kipalestina na vikosi vya Israeli.
Idadi ya hivi punde ni pamoja na watu 103 waliouawa katika muda wa saa 24 zilizopita, taarifa ya wizara ilisema, huku wengine 68,291 wamejeruhiwa kote Gaza tangu vita vilipozuka Oktoba 7.
Wakati hayo yanajiri mazungumzo ya kusitisha vita vya Israel na Hamas na kuwaachilia mateka waliosalia yameelekea katika siku ya pili mjini Cairo siku ya Jumatano, huku raia wa Gaza waliokimbia makazi yao wakijiandaa kwa shambulio linalotarajiwa la Israel kwenye kimbilio lao la mwisho la Rafah.
Chanzo cha Hamas kiliiambia AFP kwamba ujumbe ulikuwa unaelekea katika mji mkuu wa Misri kukutana na wapatanishi wa Misri na Qatar, baada ya wapatanishi wa Israel kufanya mazungumzo na wapatanishi hao siku ya Jumanne.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, mkosoaji mkubwa wa mwenendo wa Israel katika vita vya Gaza, pia alitakiwa mjini Cairo Jumatano kwa mazungumzo na Rais Abdel Fattah al-Sisi.