Takriban wawakilishi 100 wa mateka walisafiri kwa ndege hadi The Hague Jumatano kuwasilisha malalamiko ya “uhalifu dhidi ya ubinadamu” katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) dhidi ya Hamas, linaripoti AFP.
Hamas iliwateka nyara takriban mateka 250 wakati wa shambulizi lao dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo 130 kati yao bado wanazuiliwa mateka huko Gaza, kwa mujibu wa maafisa wa Israel. Ishirini na tisa kati yao wanaaminika kuwa wamekufa.
Haim Rubinstein kutoka Jukwaa la Hostages and Missing Families Forum alisema kundi la kampeni litafungua kesi dhidi ya viongozi wa Hamas katika ICC.
ICC ndiyo mahakama pekee duniani huru iliyoundwa kuchunguza makosa makubwa zaidi yakiwemo mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
“Sisi ni familia za mateka ambao wamepitia na bado tunapitia kuzimu hii mbaya,” Rubinstein alisema katika taarifa ya televisheni kutoka uwanja wa ndege wa Ben Gurion karibu na Tel Aviv.
“Tutafungua mashtaka dhidi ya wanachama wa Hamas na washirika wao na kuhakikisha kwamba wanalipa gharama kubwa zaidi kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao wanaendelea kuufanya.”