Rais wa Ghana amemtimua waziri wake wa fedha wakati wa mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri, ishara ya kimfano kabla ya uchaguzi wa mwezi Desemba ambapo mgogoro wa kiuchumi utakuwa kiini cha mijadala. Nafasi ya Ken Ofori-Atta inachukuliwa na Mbunge Mohammed Amin Adam.
Waziri wa fedha, aliyeteuliwa kushika wadhifa huo na Rais Nana Akufo-Addo alipoingia madarakani mwaka wa 2017, anakosolewa kwa jinsi alivyoshughulikia mzozo mkubwa wa kiuchumi ambao Ghana yenye utajiri wa dhahabu na mafuta imepitia tangu miongo kadhaa.
Mnamo mwaka 2022, Ghana ilikabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi katika miongo kadhaa, na mfumuko wa bei wa zaidi ya 50%, na kulazimisha mzalishaji mkuu wa dhahabu, mafuta na kakao kuchukua mkopo wa dola bilioni 3 kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa la (IMF) na kufanya marekebisho ya deni lake.
Deni la Ghana limeongezeka na, kama nchi nyingine za Kusini mwa Jangwa la Sahara, imelazimika kukabiliana na kuzorota kwa uchumi kutokana na janga la kimataifa la coronavirus na vita kati ya Urusi na Ukraine. Hata hivyo, kwa miezi kadhaa hali ya uchumi wa nchi imekuwa ikitengemaa: IMF ilitangaza mwishoni mwa mwezi wa Januari kwamba mfumuko wa bei ulikuwa umeshuka hadi 23% mnamo mwezi wa Desemba 2023 na kwamba “unakwenda katika mwelekeo sahihi”, hata ukiwa uliendelea kuwa juu.