Mahakama ya Uturuki jana iliwahukumu washtakiwa 16 kwenda jela kwa kufanya ujasusi wa shirika la kijasusi la Israel, Mossad huku kiongozi wa mtandao huo, Selcuk Kucukkaya akipokea kifungo cha miaka 26 jela.
Mahakama ya 30 ya Jinai ya Istanbul ilimhukumu Kucukkaya kifungo cha miaka 15 jela kwa tuhuma za “ujasusi wa kisiasa na kijeshi,” miaka sita na miezi minane kwa tuhuma za uchochezi, na miaka mitano kwa kupata au kusambaza data za kibinafsi kinyume cha sheria.
Mahakama iliwahukumu washtakiwa Cenk Birturk, Fatma Birturk na Musa Kus kifungo cha miaka 18 na miezi minne jela kwa makosa yaleyale, huku mshitakiwa Emre Birturk akihukumiwa kifungo cha miaka minane na miezi tisa jela kwa makosa ya kupata au kusambaza data za kibinafsi kinyume cha sheria. .
Washtakiwa wengine 11 walihukumiwa kifungo cha miaka sita na miezi mitatu kwa kusaidia katika ujasusi wa kisiasa na kijeshi. Kesi ya Serkan Ozdemirci imetenganishwa na wengine huku akiendelea kuwa huru.
Marufuku ya kusafiri yalitolewa dhidi ya washtakiwa watano waliotiwa hatiani, huku taratibu za uangalizi wa mahakama zikifanywa kwa washtakiwa waliosalia.