Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda amewashauri wanawake kujiimarisha kiuchumi ili kuwa na maamuzi katika familia huku akieleza kuwa wakiwa na fedha itakuwa ngumu kuachwa na waume zao ingawa waume ‘watakuwa na michepuko ila hawataacha njia kuu’.
Amesema hayo wakati akiongea na wanawake wajasiriamali wa kikundi cha Tujijenge cha Wilayani Mbozi akiwasisitiza kuwa wasiogope kujaribu fursa.
“Msiogope kujaribu fursa, pambaneni. Umeolewa ukiwa na hela yako na kama na wewe unatoa mchango hayo mapenzi ni next level. Maisha ya saa hizi ukikaa tu kazi yako ni kutega goli, lazima uwe na hela yako” amesema na kuongeza;
“Mkikaa mkianza kupanga jambo na wewe unachangia hata huyo mwanaume atakuwa na respect anaona hili jukwaa nikiliacha litaweza kujisimamia. Kwa muktadha huo hakuachi ovyoovyo. Ofcose atakuwa na michepuko si mnajua wale nduguzetu (wanaume) michepuko ndio habari yao. Lakini ile njia kuu itabakia palepale kwa sababu unaweza kujisimamia kwahiyo sisi kinamama tupambane kwa sababu tunaweza na tuchukue fursa kipindi hiki ambacho kiongozi wetu mkubwa ni mwanamke na huyu mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anapambana sana kutoa firsa kwa akina mama” amesema