Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.
Mbali na hayo mkutano huo umepitisha bajeti ya kiasi cha Dola za Marekani 1,842,467 kwa ajili ya maandalizi ya kongamano na maonesho hayo.
Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Katika hatua nyingine mkutano huo umetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.
Aidha, katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye pia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar umependekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.
Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara ameeleza kuwa Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo, pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikana wa nishati ya uhakika na salama.