Marekani itajenga hadi vituo vitano vya kijeshi kwa ajili ya jeshi la Somalia katika mradi unaotaka kuimarisha uwezo wa jeshi la taifa la Somalia huku kukiwa na vitisho vinavyoendelea kutoka kwa kundi lenye itikadi kali.
Waziri wa ulinzi wa Somalia na balozi wa Marekani walitia saini hati ya makubaliano mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Makubaliano hayo yanakuja wakati ambapo tume ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, inayojulikana kama ATMIS, inapunguza uwepo wake nchini Somalia.
Kambi hizo mpya zitahusishwa na Kikosi cha Danab cha jeshi la Somalia, kilichoanzishwa mwaka 2017 kufuatia makubaliano kati ya Marekani na Somalia ya kuajiri, kutoa mafunzo, kuandaa na kuwashauri wanaume na wanawake 3,000 kutoka kote Somalia ili kujenga uwezo mkubwa wa askari wa miguu ndani ya jeshi la Somalia.
Kikosi hicho kimekuwa muhimu kama kikosi cha kuchukua hatua haraka katika juhudi za kuliondoa kundi lenye itikadi kali la al-Shabab.