Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya uchimbaji wa dhahabu Shanta Gold Mine zimesaini mkataba wa kandarasi ya uchorongaji miamba yenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.08 sawa na sh bilioni 2.7 kama sehemu ya uendelezaji wa mageuzi yanayoendelea kufanywa na shirika hilo kwenye shughuli za uchorongaji.
Utiaji saini wa mkataba huo umefanyika jijini Dodoma nchini Tanzania na utadumu kwa kipindi cha miezi sita na utahusisha shughuli za uchorongaji kwa ajili ya utafiti wa madini.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa makubaliano ya kandarasi hiyo yamefunguwa njia kwa STAMICO kuingia rasmi kanda ya kati na hasa Mkoa wa Singida, kabla ya kusaini kandarasi zingine za uchorongaji Mkoani Dodoma kupitia kampuni ya Geita Greenfields Minerals Exploration Company Ltd.
“Kandarasi hii ni miezi sita na ina thamani ya dola milioni 1.08 sawa na bilioni 2.7, kandarasi amabayo sisi tunaheshimu na kupitia kandarasi hii sisi tunawahakikishia kuwapatia huduma stahili” Alisema Dkt. Mwasse