Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis, ametoa wito kwa makundi yanayopigana nchini Sudan kusitisha vita iliyodumua kwa miezi 10 hivi sasa, ambapo imesababisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao na kuzua hofu ya baa la njaa.
Akizungumza katika ibada ya kila Jumapili mjini Vatican, Papa Francis, aliziomba pande hasimu kukomesha mapigano, aliyosema yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na maafa kwa raia wasio na hatia.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa, ni imani yake kuwa viongozi wanaopigana watasikia mwito wake na kurejea katika meza ya mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu.
Wito wake unakuja wakati huu, Juhudi za kidiplomasia zikiwa zimeshindwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kati ya jeshi la Serikali na wapiganaji wa RSF.