Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema kuwa takwimu za sasa zinaonesha kuwa takribani eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta 469,000 kila mwaka linapotea nchini.
Amesema hali hiyo si nzuri na kama juhudi za pamoja hazitachukuliwa basi kasi ya kuenea kwa jangwa zitaathiri nchi na hatimaye kuchangia kwenye kuathiri dunia katika siku za usoni.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua mkakati wa Kitaifa wa Mianzi na mpango kazi wake, Kairuki amesema ili kukabiliana na hali hiyo, juhudi za kuendeleza miti ya mianzi ni jambo la muhimu na kwamba kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha misitu inaendelezwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema ni muhimu pia kwa wadau wote wa Misitu nchini kusoma kwa umakini Mkakati na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Mianzi ili kupata picha ya tulipo sasa na kuhakikisha kuwa unatekelezwa ipasavyo ili kuendeleza misitu hapa nchini.
Amewataka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha mbegu za mianzi hususani zile za kibiashara zinapatikana kwa urahisi ili wananchi na wadau wengine waweze kufikia malengo waliyojipangia.
“Ninaielekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu kufanya tafiti za kutambua maeneo sahihi ya kupanda aina mbalimbali za mianzi pamoja na kuiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ifanye tafsiri ya nyaraka hizi mbili kwa lugha ya Kiswahili na kuzisambaza. Serikali itaweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wa zao la mianzi ili kuhakikisha linaleta tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla,” amesema