Baada ya ukosefu wa kutisha wa chakula, kuongezeka kwa utapiamlo na kuenea kwa magonjwa kunaweza kusababisha mlipuko wa vifo vya watoto huko Gaza, Umoja wa Mataifa ulionya Jumatatu.
Wiki 20 baada ya vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kwamba chakula na maji salama vimekuwa “adimu sana” katika ardhi ya Palestina, na kuongeza kuwa karibu watoto wote wadogo walikuwa na magonjwa ya kuambukiza.
“Ukanda wa Gaza uko tayari kushuhudia mlipuko wa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika ambavyo vitaongeza kiwango kisichoweza kuvumilika cha vifo vya watoto huko Gaza,” alisema Ted Chaiban, naibu mkuu wa shughuli za kibinadamu katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Angalau asilimia 90 ya watoto chini ya miaka mitano huko Gaza wameathiriwa na ugonjwa mmoja au zaidi wa kuambukiza, kulingana na tathmini ya pamoja ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa watoto, chakula na afya.