Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema Taifa linahitaji Walimu bora na mahiri katika kufundisha pamoja na uwezo wa kukaa na kuwalea vizuri watoto wa Kitanzania ili wafikie malengo yao na kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali.
Profesa Mkenda aliyasema hayo Jana wilayani Korogwe Mkoani Tanga wakati akifungua Mafunzo ya Kitaifa kuhusu Uongozi, Usimamizi wa Shule na Utawala bora pamoja na kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 347, kutoka Wilaya ya Korogwe Mji, Korogwe Vijijini na Lushoto ambapo alieleza kuwa Ualimu ni moja ya taaluma muhimu na msingi mama kwa Maendeleo ya Taifa.
“Tunahitaji kuwasaidia Walimu kujiendeleza Kitaaluma, Hivyo kwenye Sera sasa hivi itakuwa ni lazima anayemaliza chuo cha Ualimu aende akafanye mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja apimwe ili aweze kuhitimu kama kada nyingine zinavyofanya” alisema Waziri Mkenda nakuongeza kuwa hawataki ualimu uvamiwe.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa mageuzi ya Elimu ndio agenda kubwa Duniani, na kwamba tayari Serikali ilishaanza kufanyia kazi mageuzi hayo ili kuendana na wakati pamoja na kukidhi mahitaji ya sasa na baadae ya Taifa na kitaifa.
Aidha amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kurudisha heshima ya Ualimu na kuhakikisha wanapata walimu wenye sifa stahiki, bora, wenye uwezo na umahiri wa kufundisha na kulea watoto kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha Walimu wanathaminiwa katika kutenda kazi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali, kununua vifaa ikiwemo vishkwambi na kuweka mazingira rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema mpaka sasa Walimu wamefanya kazi kubwa, na kwamba bado kuna kazi kubwa zaidi inawahitaji kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
” Ni ukweli usiopingika Walimu ndio tegemeo letu kubwa sana hapa Nchini, mmechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika Elimu yetu, bila nyie hatuna elimu” Alieleza Mkenda.