Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kuweka sharti kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwenye tafiti zozote nchini zinazohusisha masuala ya chakula na lishe katika Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Februari 20, 2024 wakati wa ziara yake ya kukagua na kuona kazi zinazofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe kwa upande wa Maabara iliyopo Mikocheni Jijini Dar Es Salaam.
“Tunampango wa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwa mtu yeyote au shirika lolote linalofanya tafiti zinazohusu masuala ya chakula na lishe, lazima zithibitishwe na ushahidi wa kisayansi baada ya sampuli kuchukuliwa na kuletwa katika maabara hii, isiwe tu ni tafiti za kwenye makaratasi.” Amesema Waziri Ummy.
Waziri @ummymwalimu amesema maabara hiyo ya chakula na lishe ni moja ya maabara kubwa na zinazoaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambapo amefurahishwa na kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuja na ushahidi wa kisayansi.
“Lakini pia kuna utafiti ambao wameufanya na kushauri kwamba wataalamu wa Afya wanashauri na kuelekeza watoto wa umri chini ya miezi Sita wasipewe chakula kingine chochote zaidi ya maziwa na mama”. Amesema Waziri Ummy.
Maabara hiyo imegawanyika katika sehem Tatu ambayo ni maabara ya chakula (food chemistry) ambayo inafanya uchunguzi wa viinilishe (macro and micro nutrients), maabara inayofanya uchunguzi wa viashiria vya viini lishe mwilini (micronuient biomarkers), na maabara inayofanya uchunguzi wa hali ya lishe (body composition) ikiwa ni pamoja na kugundua kama chakula kimeharibika.