Shirikisho la wenye viwanda nchini ( CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), wamezindua mipango ya ushiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Wazalishaji Tanzania 2024, Tanzania International Manufacturers Expo (TIMEXPO2024).
Maonesho hayo yamepangwa kufanyika kuanzia Septemba 26 hadi 29 , 2024 mwaka huu katika viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam ikiwa ni mara ya pili tangu CTI na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuingia makubaliano ya kufanya maonesho hayo.
Leodegar Tenga, ambaye ni Mkurugenzi wa (CTI), ameeleza matumaini yake kwa maonesho ya mwaka huu, akisisitiza lengo lake la kukuza ushirikiano kati ya wazalishaji wa ndani na wazalishaji wa kimataifa.
Akizungumzia kauli mbiu ya “Kujenga Daraja na kukutanisha wazalishaji wa ndani na Nje,” Tenga aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuinua uzalishaji wa ndani hadi kuwa na viwango vya kimataifa.
Fortunatus Mhambe ambaye ni Mkurgenzi wa Kukuza Biashara TANTRADE, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa (TANTRADE), alionesha umuhimu wa kuunganisha viwanda vya ndani na vya nje na kueleza jukumu la tukio hilo katika kurahisisha kubadilishana maarifa na maendeleo ya kiteknolojia, muhimu kwa kuweka viwanda vya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
Pia Mhambe aliwahimiza wadau kushiriki kikamilifu, kwani zaidi ya makampuni 500 kutoka masoko ya ndani na kimataifa yanatarajiwa kushiriki kwa kuonyesha bidhaa na huduma zao.