Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na washirika wake wa kibinadamu wametoa ombi la dola bilioni 2.6 za Kimarekani ili kufadhili mpango wa kutoa misaada ya kibinadamu wa mwaka 2024 nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Jumanne na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA), fedha hizo zinalenga kutoa msaada wa kuokoa maisha na ulinzi kwa watu milioni 8.7 wenye uhitaji.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, mzozo wa kibinadamu nchini DRC umefikia viwango vya kutisha, huku ongezeko jipya la ghasia, hasa mashariki mwa nchi hiyo, likiwalazimisha waathirika kuyahama makazi yao.
Mratibu Mkazi na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Bruno Lemarquis amesema mgogoro wa kibinadamu nchini DRC umefikia hatua mpya mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa mizozo, kuibuka kwa mivutano mipya, na majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
Kutokana na hali hii, kuna wanaume, wanawake na watoto wanaokabiliwa na mazingira magumu sana.