Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kwa kufanikiwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya shilingi bilioni 29.5 sawa na asilimia 134 katika kipindi cha mwaka 2022/2023.
Kanali Thomas ametoa pongezi hizo wakati anazungumza kwenye ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amesema TRA katika kipindi hicho wamefanya kazi nzuri ya kukusanya mapato kwa kuwa wamevuka lengo la makusanyo ya zaidi ya shilingi bilioni 21 ambapo amesema Uchumi wa Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuimarika.
“Mkoa unaendelea kuimarika kiuchumi kwa kuimarika kwa miundombinu,shughuli za uzalishaji mali,biashara na ukewekezaji shughuli za uchimbaji madini hasa makaa ya mawe,maboresho ya uwanja wa Ndege wa Songea na biashara na nchi jirani za Msumbiji na Malawi’’,alisistiza RC Thomas.
Ameyataja mazingira ya kujifunzia na kufundishia wanafunzi yamekuwa bora zaidi ambapo Mkoa uliletewa fedha za kujenga shule mpya 12 za msingi kupitia BOOST kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 7,7 pia serikali ilileta fedha zaidi ya shilingi bilioni tano kujenga sekondari mpya tisa kupitia program ya SEQUIP.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 serikali imetoa shilingi milioni 900 kukarabati hospitali kongwe ya Tunduru na zaidi ya shilingi bilioni tatu zimetolewa na serikali kujenga hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma katika eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea.