Mlipuko mkali wa kipindupindu kwa sasa umesababisha kero kubwa jamii za nchi za Kusini mwa Afrika, katika kile ambacho wataalam wanasema ni janga mbaya zaidi kulikumba eneo hilo kwa zaidi muongo mmoja.
Maelfu ya watu wamekufa, na maelfu ya wengine wameambukizwa na ugonjwa huo wa kuhara katika angalau nchi saba. Katika baadhi ya nchi zilizoathiriwa zaidi, milipuko hiyo ililazimisha mamilioni ya wanafunzi kusalia nyumbani mnamo Januari.
Katika eneo lote, vituo vya kukabiliana na dharura vimechipuka katika uwanja wa shule na viwanja vya michezo, na vimejaa wagonjwa wanaougua kwa maumivu. Hofu inaongezeka kwamba ikiwa milipuko hiyo haitashughulikiwa hivi karibuni, wafanyikazi wa afya wanaweza kuzidiwa.
Katika wito wa dharura wa kushughulikia mlipuko huo mapema mwezi huu, viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walisema wanajitahidi kukomesha kuenea, lakini ukosefu wa maji safi, ukaguzi dhaifu wa mipaka, na uhaba wa chanjo ulimwenguni ni mambo yanayoweza kuvuriga azma hiyo.
Tangu Januari 2022, takriban watu 188,000 wameambukizwa kipindupindu katika nchi saba za SADC ambazo ni Zambia, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Tanzania, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Zaidi ya watu 4,100 wamefariki dunia, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu, OCHA.