Kufuatia tangazo kwamba Thomas Tuchel atajiuzulu kama kocha mkuu msimu huu wa joto, Bayern Munich sasa wanatafuta mbadala wake na kwa mujibu wa Sky Germany, kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso anaonekana kuwa mgombea bora wa mabingwa hao wa Ujerumani.
Mchezaji huyo wa zamani wa Bayern amefanya maajabu tangu achukue mikoba ya Leverkusen Oktoba 2022, na timu yake kwa sasa ipo kileleni mwa Bundesliga, pointi nane mbele ya The Bavarians.
Mkurugenzi wa zamani wa ufundi wa Bayern, Michael Reschke alisema katika mahojiano mwezi uliopita kwamba Bavarians walikuwa na nia ya kumwajiri Mhispania huyo kama mkurugenzi wa michezo wakati maisha yake ya uchezaji yalipomalizika 2017.
Hata hivyo, Mhispania huyo alikuwa na mipango mingine na akaendelea kufundisha katika ngazi ya vijana, kwanza akiwa Real Madrid na baadaye Real Sociedad, kabla ya kujiunga na Leverkusen.
Mkataba wake na Leverkusen unamalizika 2026, lakini inatia shaka kama atakaa muda huo, huku Liverpool pia ikiripotiwa kutaka kumwajiri.