Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tanga kuchukua hatua za mapema katika kukabiliana na changamoto ya soko la matunda yanayozalishwa mkoani humo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kabuku Wilaya ya Handeni akiwa ziarani mkoani Tanga leo tarehe 21 Februari 2024. Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kufanya tathimini na kutambua kiasi cha matunda yanayozalishwa katika eneo hilo.
Aidha Makamu wa Rais amemuagiza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kukutana na wamiliki wakubwa wa viwanda vya kuchakata matunda (Bakhresa na Jambo Product) ili waweze kutumia matunda yanayozalishwa Wilaya ya Handeni na Tanga kwa ujumla katika bidhaa zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kabuku na Watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Amesema athari za uharibifu wa mazingira zimepelekea ongezeko la joto kupita kiasi, ongezeko la mvua ambayo imepelekea uharibifu wa miundombinu na mlipuko wa magonjwa.
Amesema ni muhimu watanzania kutambua uhifadhi ya mazingira ni jukumu la kila mmoja kwa kuacha kukata miti ovyo, kuacha kuchoma misitu pamoja na kupanda miti na kuitunza.