Mamlaka nchini Malawi imesitisha utoaji wa hati za kusafiria kufuatia shambulio la mtandaoni kwenye mfumo wa kompyuta katika idara ya uhamiaji nchini humo.
Rais Lazarus Chakwera aliwaambia wabunge kwamba hatua hiyo ya kulengwa kwa idara ya serikali ni sawa na “ukiukaji mkubwa wa usalama wa taifa”.
Aidha rais Chakwera alieleza kuwa wadukuzi hao walikuwa wakiomba fidia suala ambalo amesisitiza kwamba halitakubalika na kwamba serikali inajitahidi kutatua tatizo hilo.
Idadi kubwa ya watu nchini Malawi wamekuwa wakitatfuta hati za kusafiria , vijana wengi wakitafuta wakiwa na nia ya kuondoka kwenye taifa hilo kutafuta maisha bora katika nchi za kigeni.
Rais Chakwera alisema ameipa idara ya uhamiaji muda wa wiki tatu ambapo inatakiwa kutoa suluhu la muda na kuanza tena utoaji wa hati za kusafiria, huku wakisubiri kurejesha udhibiti wa mfumo huo.