Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), wametia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) ya Zanzibar, lengo ni kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi ili kuzalishaji nguvu kazi yenye ujuzi mahiri sambamba na mabadiliko ya sera ya elimu na mitaala. Mabadiliko haya yanahusisha uanzishwaji wa mchepuo wa Mafunzo ya Amali kuanzia ngazi ya Sekondari, hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya walimu wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi.
Makubaliano ya ushirikiano huo yamesainiwa leo, tarehe 21 Februari, 2024 visiwani Zanzibar, kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Prosper Mgaya, na Mkuu wa KIST, Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, na kushuhudiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano, ushirikiano huo utajikita katika kubadilishana taarifa za uandaaji na utekelezaji wa mitaala ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi; kuendesha programu za kubadilishana wakufunzi, vifaa vya kufundishia na nafasi za mazoezi kwa vitendo kwa wanafunzi; kufanya utafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi, pamoja na uandishi na utekelezaji wa miradi yenye kuboresha utoaji wa Elimu na mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Bi. Lela Mohamed Mussa, amesema ushirikiano huo ni muhimu sana na utakuwa kichocheo katika kuwezesha utekelezaji wa Mabadiliko ya Sera ya Elimu (Majereo 2023) kuhusu Mafunzo ya Amali ambapo walimu mahiri wanatakiwa ili kutoa mafunzo hayo kwa ufanisi.