Rwanda imetupilia mbali tuhuma za Ufaransa kwamba inawaunga mkono waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao za mauaji na uharibifu katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alisema katika taarifa yake iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii kuwa:.”Katika taarifa ya Serikali ya Ufaransa kuhusu hali ya mashariki mwa DRC tunaweza kusima hivi, hakuna anayejua zaidi kuhusu sababu na historia ya mzozo wa mashariki mwa DRC kuliko Ufaransa. ”
Makolo alisema kuwa kushughulikia masuala ya msingi itakuwa muhimu katika kutatua mzozo unaoendelea.
Ufaransa hapo awali iliitaka Rwanda kusitisha “uungaji mkono” wowote kwa waasi wa M23 na kuondoa wanajeshi wake kutoka mashariki mwa DRC.
Huku kukiwa na madai yanayodokeza kwamba kundi la M23 kimsingi lina wapiganaji wa Kitutsi wa Rwanda, Kigali imekanusha mara kwa mara madai ya kuunga mkono kundi hilo. Idadi ya Watutsi wa Kongo ni asilimia ndogo (1-2%) ya watu wote wa DRC.
Katika taarifa ya hivi majuzi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilihusisha harakati za kivita za hivi karibuni za M23 na hatua ya serikali ya DRC kufukuza kwa Jeshi la Kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki na DRC mnamo Desemba 2023. Rwanda inasema kufukuzwa huko kulivuruga juhudi za usitishaji mapigano na mchakato wa uondoaji, na kusababisha kuongezeka kwa migogoro.