Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema wameona madai ya kuaminika kwamba wanawake na wasichana wa Kipalestina wamefanyiwa unyanyasaji wa kingono, ikiwa ni pamoja na ubakaji, wakiwa kizuizini Israel, na wanataka uchunguzi kamili ufanyike.
Jopo hilo la wataalamu lilisema kuna ushahidi wa angalau visa viwili vya ubakaji, sambamba na visa vingine vya udhalilishaji kingono na vitisho vya ubakaji. Reem Alsalem, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, alisema kiwango cha kweli cha unyanyasaji wa kingono kinaweza kuwa kikubwa zaidi.
“Huenda tusijue kwa muda mrefu idadi halisi ya wahasiriwa ni nini,” alisema Alsalem, ambaye aliteuliwa kuwa mwandishi maalum na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) mnamo 2021.
Alibainisha kuwa kusitasita kuripoti unyanyasaji wa kijinsia ni jambo la kawaida kwa sababu ya hofu ya kulipizwa kisasi dhidi ya waathiriwa.
Alisema kuwa katika wimbi la kuzuiliwa kwa wanawake na wasichana wa Kipalestina baada ya kuzuka kwa vita vya Israel na Hamas tarehe 7 Oktoba, kulikuwa na mtazamo unaozidi kuruhusu unyanyasaji wa kijinsia katika vituo vya wafungwa vya Israel.