Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu waliojiunga na program ya mafunzo tarajali katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), kujituma kwa bidii, kuwa wabunifu na nidhamu.
Pia ametoa wito kwa wahitimu hao, kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya mgodi huo ili kujiendeleza na kuondoka wakiwa tofauti na namna walivyoingia kwenye program hiyo ya mwaka mmoja.
Shigela ametoa wito huo hivi karibuni mjini Geita katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo vikuu ambao wamejiunga na GGML kwa mwaka 2024/2025 kupata mafunzo tarajali sambamba na wahitimu wengine 10 wa program hiyo kwa mwaka jana ambao wameendelea na mafunzo ya juu zaidi baada ya kupata ajira ya kudumu ndani ya GGML.
Wanafunzi hao 10 waliomaliza program mwaka jana, wamechaguliwa kuendelea na program mpya inayofahamika kwa jina la African Business Unit Graduate (ABU) ambayo inawapa fursa ya kubadilishana uzoefu na wahitimu wa aina hiyo katika nchi nyingine za Ghana na Guine ambako AngloGold Ashanti kampuni mama ya GGML inamiliki migodi.
Shigela alisema nidhamu kwa wahitimu hao ni msingi muhimu katika utumishi wa aina yoyote hivyo wanapaswa kuzingatia nidhamu katika utendaji wao na hata wanapokengeuka kutekeleza majukumu yao nafsi inapaswa kuwasuta.
Alisema lengo la program hii ni kuwaandaa wafanyakazi wabobezi ambao wanaweza kuja kuwa viongozi wa baadae wa kampuni hiyo na hata nje ya GGML.