Jimbo la Kavuu lililopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi katika kipindi cha kuanzia Novemba 2020 mpaka Februari 2024 limefanikiwa kutekeleza miradi ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Tsh 9,986,388,189.47.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu wa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024. Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Amesema, kati ya kiasi hicho cha fedha Tsh 6,849,553,942.86 zimetumika kujenga miundombinu ya madarasa, kukamilisha maboma, maabara na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari huku Tsh 1,258,714,246.61 zikutumika kugharamia elimu bila malipo, mitihani na kulipa posho kwa walimu wanaojitolea wa masomo ya sayansi.
Aidha, Mhe, Pinda alisema katika kipindi hicho cha utekelezaji ilani ya CCM jimbo lake la Kavuu limeweza kuimarisha utoaji wa elimu Jumuishi kwa wanafunzi ambapo ndani ya jimbo hilo kuna shule 27 jumuishi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kitengo kimoja kilichopo shule ya msingi Majimoto.
‘’ Jumla ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 219 yaani wavulana ni 133 Wasichana 86 na walimu 10 wakiwemo wanaume 6 na wanawake 4 na miundombinu inaendelea kuboreshwa kuhakikisha makundi yote ya watoto wanapata haki ya kupata elimu na katika mazingira wezeshi’’ alisema Mhe, Pinda.