Mahakama moja nchini Tunisia imemuhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Moncef Marzouki kifungo cha miaka 8 jela kwa kosa la kujaribu kuzusha machafuko nchini Tunisia. Hukumu hiyo imetolewa bila ya Marzouki kuwepo mahakamani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, mahakama ya mwanzo nchini Tunisia imemhukumu rais huyo wa zamani wa nchi hiyo ambaye ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa rais wa hivi sasa wa Tunisia, Kais Saeed, kifungo cha 8 jela bila ya kuwepo mahakamani. Lakini hukumu hiyio dhidi ya Marzouki imelalamikiwa vikali kwa kukandamiza wapinzani kwa madai kama ya kuzusha machafuko nchini Tunisia.
“Mohammed Zaitouneh,” msemaji rasmi wa Mahakama ya Mwanzo ya Tunisia, ameviambia vyombo vya habari kwamba, rais huyo wa zamani wa Tunisia amehukumiwa kifungo cha miaka 8 jela kwa tuhuma za kujaribu kubadilisha muundo wa serikali na kusababisha machafuko kupitia kuwachochea watu kuanzisha vita vya kutumia silaha.
Marzouki, ambaye kwa sasa anaishi nchini Ufaransa, alikuwa rais wa kwanza wa Tunisia kuingia katika ikulu ya nchi hiyo kwa njia ya demokrasia baada ya mapinduzi ya 2011 yaliyomg’oa madarakani dikteta Ben Ali.