Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA) linafanya mkutano wake jijini Nairobi Kenya na kujadili jinsi mataifa ya duniai yanavyoweza kushirikiana kukabiliana na migogoro kama vile mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa viumbe hai.
Kabla ya mkutano huo, Mkuu wa Mpango wa Kimataifa wa Mazingira (UNEP), Inger Andersen, aliziambia duru za habari kwamba, hakuna binadamu yeyote anayeishi peke yake na kwamba kila mtu anaishi katika sayari ya dunia.
“Kila mmoja lazima ashirikishwe kwa kuwa njia ya pekee ya kutatua baadhi ya matatizo hayo ni kwa mazungumzo ya pamoja.” Alisema.
Mkutano huo katika mji mkuu wa Kenya ni kikao cha sita cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kinachohudhuriwa na nchi wanachama, mashirika ya kiraia, wadua wa mazingira, wanasayansi na sekta binafsi.
Katika mkutano huo, nchi wanachama hujadili rasimu za maazimio kuhusu masuala mbalimbali ambayo baraza hilo hupitisha baada ya makubaliano.
Mkutano huo unafanyika huku mataifa ya pembe ya Afrika ikiwemo Kenya na Somalia hivi karibuni yalikabiliwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.