Makumi ya watu wameuawa kwa kupigwa risasi wakiwa msikitini baada ya kanisa kushambuliwa,mamlaka nchini Burkina Faso zinasema.
Ilikuwa wakati wa sala ya asubuhi ambapo watu wenye silaha waliuzingira msikiti katika mji wa Natiaboani.
“Waathiriwa wote walikuwa Waislamu, wengi wao wanaume,” mkazi wa eneo hilo aliambia shirika la habari la AFP.
Zaidi ya theluthi moja ya Burkina Faso kwa sasa iko chini ya udhibiti wa wanamgambo wenye itikadi kali.
Washambuliaji hao wanashukiwa kuwa wapiganaji wa Kiislamu ambao pia waliwalenga wanajeshi na wanamgambo wa kujilinda waliokamatwa siku hiyo hiyo.
Vyombo vya habari vya ndani vinaelezea (kwa Kifaransa) kuhusu uvamizi mkubwa wa mamia ya wanamgambo wenye bunduki waliokuwa wakitumia pikipiki.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha kuwa idadi ya waliokufa kutokana na shambulio la msikiti inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ile iliyotolewa na maafisa.
Natiaboani, ambapo mashambulizi hayo yalitokea, iko katika eneo la mashariki mwa Burkina Faso ambako makundi mengi yenye silaha yanaendesha shughuli zake.
Siku hiyo hiyo, waumini wasiopungua 15 waliuawa katika shambulio dhidi ya kanisa katoliki wakati wa misa ya Jumapili huko Essakane kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.