Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Awamu ya Sita, mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji yameimarika na kuwa bora zaidi kwa kipindi kifupi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa mwaka 2024 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara licha ya misukosuko ya uchumi na kijamii inayoendelea Duniani kote.
Ameongeza kwamba katika mwaka 2023, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuwa 5.0% ikilinganishwa na 4.7% mwaka 2022 huku matarajio kwa mwaka 2024 ni ukuaji wa 5.5%.
Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa Jukwaa hilo kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru ili kuweza kuboresha vema sera za kodi na uwekezaji nchini. Amesema maoni yatakayotolewa katika Jukwaa hilo yatatumika katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Aidha amewataka Mawaziri wa Fedha kuzingatia ushauri wa sekta binafsi na walipa kodi wote ili wadau waone umuhimu wa ushiriki wao katika jukwaa hilo.
Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki kujikita katika kuibua njia za kibunifu zitakazosaidia kuongeza mapato ya Serikali bila kuumiza Wafanyabiashara na Wawekezaji. Amewataka kujadiliana kwa kina kuhusu namna ya kutumia zaidi ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, mathalan kupitia hatifungani zitakazotolewa na taasisi na mashirika ya umma kugharamia miradi ya maendeleo.
Pia amewasihi mijadala kujielekeza katika kubaini na kudhibiti vihatarishi vya matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ikiwemo wizi wa kimtandao na utoroshaji wa mitaji.