Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani umegundua kuwa kuvuta au kula bidhaa zozote zenye bangi husababisha athari kubwa kwenye moyo wa Binadamu kama vile kupata mshtuko wa moyo pamoja na kiharusi na yote haya hutokea hata kama Mtu hakuwa na magonjwa ya moyo na hajawahi kuvuta sigara hapo zamani.
Utafiti huo pia uligundua kuwa hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi kwa wanaotumia bangi kila siku ya maisha yao uliongezeka kwa 42% na hatari ya mtu kupata mshtuko wa moyo pia kwa anaevuta kila siku iliongezeka kwa 25% ambapo liliongezeka kadri idadi ya siku za matumizi ya bangi zilivyoongezeka.
Robert Page II, Profesa wa Chuo Kikuu cha Colorado Skaggs School of Pharmacy na Sayansi ya Madawa huko Aurora, Colorado alisema ongezeko la matumizi ya bangi yamehusishwa na mshtuko wa moyo pamoja na ugonjwa na kiharusi ambapo Vijana wa makamo walio chini ya miaka 55 na Wanawake chini ya umri wa miaka 65 ambao walitumia bangi walikuwa na hatari kubwa ya 36% kupata magonjwa ya moyo, mshtuko wa moyo na kiharusi bila kujali kama walitumia pia bidhaa za kitamaduni za tumbaku kama vile sigara.
Taasisi ya magonjwa ya Moyo nchini Marekani inawashauri Watu kujiepusha na uvutaji wa sigara na bangi au kula vyakula vilivyowekewa bangi ikiwa ni pamoja na bidhaa za bangi kwa sababu ya madhara yanayoweza kutokea kwenye moyo, mapafu na mishipa ya damu.