Kocha mpya wa Yanga, Marcio Maximo amefungua ukurasa mpya na kipa Juma Kaseja na kuiaidi kuing’arisha timu hiyo kimataifa kama ilivyo TP Mazembe, wakati kiungo Mbrazili, Andrey Coutinho akitua nchini jana tayari kujiunga na vigogo hao.
Maximo na msaidizi wake, Leonardo Leiva, waliowasili nchini juzi Alhamisi, kila mmoja amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha klabu hiyo.
Kocha huyo raia wa Brazil anarithi nafasi ya Mdachi Hans Van Der Pluijm, aliyeifundisha Yanga kwa miezi sita kisha kutimkia Saudi Arabia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Maximo alisema: “Nataka Yanga ifanane na ukubwa wa historia yake, Yanga iwe klabu inayowika siyo tu ndani ya Tanzania bali Afrika.
“Leo hii kila mtu ulimwenguni anaifahamu TP Mazembe kwa sababu ya mafanikio iliyoyapata, hivyo ndivyo nataka Yanga iwe.”
Akimzungumzia kipa Kaseja, ambaye walikuwa ‘paka na panya’ baada ya kukorofishana wakati akiinoa Taifa Stars, Maximo alisema hana tatizo na Kaseja, yaliyopita yamepita na hawakuwa na ugomvi, yalikuwa makubaliano, ambapo hata hivyo hakuweka wazi makubaliano waliyokuwanayo.
Maximo aliongeza: “Kaseja ni kipa bora hapa nchini na naamini ataisaidia Yanga akishirikiana na wengine waliopo kama huyu Dida (Deogratias Munishi).”
Pia, alisema amewasilisha ombi kwa uongozi wa Yanga akitaka apewe fursa ya kusajili wachezaji makini kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kuhakikisha lengo lake la kuifanya klabu bora linafanikiwa.
Kuhusu mikakati yake, alisema ataanza rasmi kuinoa timu hiyo Jumatatu ijayo kwa kuanza na progamu ya mazoezi ya kujenga stamina, kisha kuhamia katika mbinu na ufundi.
Wakati huohuo, Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Andrey Coutinho ametua nchini jana na kuahidi kuifanyia mambo makubwa klabu hiyo.
Coutinho alitua Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere majira ya saa 8:00 mchana na kupokelewa na viongozi wa Yanga wakiwamo Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohamed Binda, Ofisa Habari, Baraka Kizuguto na Meneja Hafidh Saleh.
Coutinho alisema amekuja Tanzania kwa lengo moja kuhakikisha Yanga inafanya vizuri na amejiandaa kwa changamoto zote, amezoea kupambana ingawa ameomba ushirikiano kwa mashabiki hao, uongozi na wachezaji wenzake.
Source: Mwananchi